Ofisi ya Makamu wa Rais, imesema imeendelea kuweka mikakati na mipango mahsusi ili kuhakikisha inarejesha uoto wa asili katika ardhi takribani hekta milioni 5.2 ifikapo 2030.

Hayo yamesemwa leo Novemba 6, 2023 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga wakati akifungua warsha ya Programu ya Urejeshaji ya kidunia (TRI), kutoka mataifa 10 duniani inayotekeleza Mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai ulimwenguni.

Amesema uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea maliasili ikiwemo misitu, bahari,maziwa, mito, ardhi oevu, wanyamapori na ardhi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini, hata hivyo matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali hizo yameleta tishio la uwepo wa rasilimali hizo.

“Upotevu wa bioanuai ikiwa ni pamoja na viumbe wengine wa majini unachochewa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu ikiwemo kilimo na matumizi mengine ya ardhi yasiyo endelevu. Tumeanzisha programu mbalimbali za urejeshaji wa uoto wa asili ikiwemo kampeni ya upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali ya nchi,” amesema Maganga.

Inakadiriwa duniani kote takribani ekari milioni 18.7 za misitu hupotea kila mwaka na kutokana na umuhimu wa urejeshaji wa ardhi, na Tanzania imetenga ukubwa wa eneo takriban asilimia 40 ya eneo lote la ardhi ikijumuisha 6.5% ya bahari na 33% ya maeneo ya nchi kavu.

Dkt. Biteko ashiriki mazishi ya kaka wa Majaliwa
Vision 2030 kugusa maisha ya Mtanzania wa kawaida