Imefahamika kuwa Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira Robertinho’ anatajwa kukalia kuti kavu kutokana na matokeo ya mechi iliyochezwa juzi Jumapili (Novemba 05) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Simba SC ilipoteza mchezo huo wa mzunguuko wa nane wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufungwa na Young Africans mabao 5-1, na kuleta taharuki kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kongwe nchini Tanzania.

Taarifa zilizotolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC ambaye hakutaka jina lake kuanikwa hadharani zinaeleza kuwa, Robertinho yupo katika Presha ya kupoteza kibarua baada ya kichapo hicho.

Mjumbe huyo amesema baada ya mchezo dhidi ya Young Africans, kundi kubwa la viongozi wenye ushawishi Simba SC wakiwemo wale ambao awali walikuwa wanamuunga mkono Robertinho, linaonekana kupoteza imani naye na linatoa ushauri kuwa awekwe kando.

“Kuhusu uamuzi wa kumtimua bado haujafanywa na wala hatujakaa kuzungumzia hilo kama inavyoandikwa mitandaoni. Tumeona tuwe watulivu kwa sasa ili tusifanye uamuzi wa presha lakini kiuhalisia nafasi ya kocha kubaki ni finyu,” amesema mmoja wa viongozi wa Simba SC.

Tangu alipotua nchini mwanzoni mwa mwaka huu, Robertinho amepoteza mchezo mmoja wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans, huku akiifikisha timu hiyo Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu uliopita 2022/23.

Msimu huu ameipeleka timu hiyo hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuitoa Power Dynamos ya Zambia, huku akionesha upinzani mkali dhidi ya Al Ahly ya Misri kwenye michuano ya African Football League.

Hadi sasa ameiongoza Simba SC katika michezo saba ya Ligi Kuu msimu huu 2023/24, akishinda michezo sita akipoteza mchezo mmoja dhidi ya Young Africans.

Wakandarasi wazawa wanashiriki Ujenzi Bomba la Hoima - Kapinga
Barcode: Wajasiriamali walia na TBS, Malisa awatuliza