Baada ya kuibanjua Tanzania Prisons kwa mabao 2-1, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Mecky Maxime amesema wataendelea na mazoezi yao kama kawaida kwa ajili ya kujiweka fiti katika kipindi hiki cha michezo ya kimataifa.

Maxime amesema ushindi huo ulikuwa ni muhimu kwao baada ya kushindwa kutamba katika michezo miwili mfululizo ila jambo analoendelea kukabiliana nalo ni kutengeneza uwiyano wa timu kwenye uzuiaji na ushambuliaji.

“Sio kwa kiwango kikubwa kwa sababu tulishinda ila tunaendelea kuruhusu mabao japo ushindi ndio lengo la kwanza kwetu, tunahitaji mwendelezo wa hilo ili kutengeneza uwiyano kwenye timu itakayotusaidia katika kila mchezo wetu,” amesema.

Maxime ambaye huo ulikuwa ni ushindi wake wa tatu Ligi Kuu Tanzania Bara katika michezo tisa aliyocheza msimu huu 2023/24, ameeleza lengo kubwa la timu hiyo ni kushika nafasi tano za juu na hilo litawezekana endapo tu watakuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo.

“Kila mmoja wetu ana malengo yake aliyojiwekea na hivyo pia kwetu, msimu huu umeanza na ushindani kwa sababu timu zote zimejipanga vizuri, kadri ambavyo ligi inazidi kusonga ndivyo ugumu nao unaongezeka hivyo ni muhimu kujiandaa mapema.”

Kikosi hicho kitakuwa tena na kibarua kingine kigumu Novemba 22, kwenye Uwanja wake wa Kaitaba itakapoikaribisha KMC FC.

Kocha Singida FG akiri mambo magumu
Ally Kamwe: Tutaipiga Al Ahly Ligi ya Mabingwa