Waziri wa Madini, Anthony Mavunde hii leo Novemba 8, 2023 wakati wa mazungumzo ya ushirikiano wa kisekta baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini yaliyofanyika jijini Dodoma, amesema Tanzania imefungua milango ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa nchi ya Korea ya Kusini, ikiwemo kuendeleza ushirikiano wa kikazi katika kufanikisha utekelezaji wa mikakati ya Vision 2030 ya Madini, Maisha na Utajiri.
Amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini mkakati kama vile madini ya kinywe, lithium , Nibioum na Makaa ya mawe ambayo kwasasa mataifa mengi yanatafuta kuwekeza huko kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Waziri Mavunde, pia amezikaribisha kampuni mbalimbali kutoka Korea ya Kusini kuja kuwekeza Tanzani na kuwaeleza kuwa kwasasa sekta ya madini nchini Tanzania ipo na vision2030 ambayo lengo lake ni kupata taarifa za utafiti ambazo zitatoa dira ya uwekezaji na uendelezaji kwa kufungamanisha sekta za kiuchumi.
Kuhusu kufungua kiwanda cha uchakataji madini ya kinywe na uongezaji thamani madini nchini Tanzania, Mkurugenzi wa Kampuni ya POSCO ya nchini Korea Ji Ki Chun amesema baada ya kukamilisha uchimbaji wa madini ya kinywe wilayani Mahenge watafungua kiwanda cha kuchakata madini ghafi ya Kinywe na uingezaji thamani kabla ya kusafirisha nje ya nchi.
Chun amefafanua kuwa menejimenti ya POSCO imeridhika na hali ya miundombinu nchini ikiwemo reli ya kati pamoja ujenzi wa SGR, huku Balozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania Kim Sumpyo akiipongeza Serikali kwa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Korea Kusini.
Awali, akifungua mazungumzo hayo ya ushirikiano Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ameimshukuru Balozi wa Korea kusini nchini Tanzania kwa uwekezaji mzuri katika sekta ya madini akitolea mfano uwekezaji katika madini ya Kinywe wilayani Mahenge.