Scolastica Msewa, Chalinze – Pwani.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani, limepitisha ujenzi wa Hoteli ya hadhi ya nyota tano na kituo cha kuuza mafuta (Petrol Station), ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuongeza vyanzo vya mapato vya Halmashauri hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 ya kuanzia mwezi julai hadi septemba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Hassani Mwinyikondo amesema miradi hiyo itaongeza mapato katika halmashauri hiyo kwani dhamira ya serikali ni kuongeza vyanzo vya mapato ili kujitegemea.

Amesema, “tayari tumefanya mazungumzo na shirika la Nyumba NHC tumekubaliana maana tunataka tuwekeze mradi wa Hoteli yenye ukumbi wa Kisasa wao wamekubali kutujengea Hoteli ya hadhi ya nyota tano hapa kwetu Chalinze, hivyo sasa tumekuja kupitisha kwenye Baraza la Madiwani leo, ili hatimaye ujenzi uanze tuwe na kiwango kikubwa cha mapato.”

Mwinyikondo ameongeza kuwa, Halmashauri ya Chalinze inalipa katika Petrol Station ya kawaida kwa robo mwaka zaidi ya milioni 90, hivyo umiliki wa Kituo hicho cha Mafuta utasaidia kuokoa fedha wanazolipa kwa wazabuni na mapato hayo yataingia moja kwa moja Halmashauri ya Chalinze.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Radhamani Possi amesema fursa nyingi zinafunguka Chalinze kwasababu ya ukaribu wake na bandari kavu ya Kwala ambapo wawekezaji wengi wanakwenda Chalinze kuwekeza lakini miundombinu ya kuwawezesha wawekezaji haikuwa ya kutosha, hivyo walitafuta wabia watakaoendesha nao miradi.

“Tumepata Wabia, hivyo tulifikisha hili kwenye baraza ili kupata ridhaa ya kuanza mchakato sasa wa kufanya maandalizi ya jumla ya ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kujua gharama ya ujenzi wake itagharimu kiasi gani na kuangalia makubaliano mengine kisha tutarudi kwenye baraza kuomba kupitishiwa maamuzi hayo” alifafanua Possi.

RC Malima ampa mwezi mmoja Mkurugenzi Kilombero
Kibu Denis: Siamini katika kubebwa, ninapambana