Polisi Kata wa Kata ya Lumemo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Edwin Kipimo ameendelea kuwafikia Wananchi kwa kutumia usafiri wa Baiskeli, kwa lengo la kutoa elimu juu ya kutambua vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia, huku Polisi kata wa kata ya Ruanda Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Happy Lumbe akiwataka Wanafunzi kuacha tamaa ya vitu vidogo vidogo kama Chips na Kuku.
Kipimo aliwatembelea watoto wa shule ya Awali, Wahudumu wa baa pamoja na Wamama waliopo katika kitongoji cha Lumemo kata ya Lumemo wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro na kuwapa elimu juu ya namna ya kutambua vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na mahali sahihi pa kutoa taarifa.
Naye, Polisi kata wa kata ya Ruanda Mkaguzi msaidizi wa Jeshi la Polisi, Happy Lumbe yeye alizungumza na Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya kutwa ya Lumbila na kuwataka kuacha tamaa ya vitu vidogo vidogo kama Chips na Kuku kutoka kwa watu wasio wafahamu, ili kuepukana na mimba za utotoni.
Sambamba na hatua hiyo, pia Mkaguzi Lumbe aliwaambia wanafunzi hao wasiogope kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto, kwani Polisi ni marafiki na ni rafiki wa watoto na wanafunzi, ujumbe ambao aliwapa wakati akitoa elimu ya Ushirikishwaji wa Jamii juu ya vitendo vya ukatili katika shule hiyo.