Mshambuliaji wa SSC Napoli, Victor Osimhen, amefunguka kuwa, uamuzi alioufanya wa kukataa kutua katika klabu za Saudi Arabia mwanzoni mwa msimu huu, ulikuwa bora kwa maisha ya soka.
Nyota huyo raia wa Nigeria, aliyeripotiwa kuwa na thamani ya pauni milioni 173 (zaidi ya sh. bilioni 431), alihusishwa kuwa mbioni kutimkia Al Hilal ya Ligi Kuu Saudi Arabia.
Osimhen mwenye umri wa miaka 24, aliyefunga mabao 31 katika mashindano yote msimu uliopita, alisaidia SSC Napoli kushinda taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Kadri nilivyowaambia hapana, ndiyo walivyokuwa wakizidisha. Ile wiki ilikuwa ni ya uamuzi mkubwa kwangu, lakini kila kitu, niliweka mikononi mwa Mungu,” alisema.
Nyota huyo alisema ofa hiyo ilikuwa kama ndoto kwake, lakini alizungumza na viongozi wake pamoja na klabu yake ya SSC Napoli.
“Hawakuwahi kukata tamaa hadi mwisho wa dirisha lao la usajili (Saudi Arabia). Nilisema kabla sijacheza mchezo wangu wa kwanza msimu huu, kiukweli sitaki kurudi nyuma kufikiria kwamba ingebadili maisha yangu.
Lakini ilibidi kufanya uamuzi ambao ni mzuri kwa maisha yangu ya soka, ingawa tunacheza mpira kwa ajili ya fedha,”
Mnigeria huyo msimu uliopita akiwa nafasi tano katika orodha ya wafungaji bora Barani Ulaya.
Kutokana na ubora wake msimu uliopita, straika huyo pia alihusishwa kuwaniwa na klabu za Manchester United na Chelsea ambazo zote ni kutoka England.