Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amemaliza ziara ya kikazi ya Siku Tatu katika Mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo pamoja na kukagua miradi ya umeme na Gesi Asilia, alisikiliza kero za wananchi na kuzitolea ufumbuzi katika Kikao cha Majumuisho ya ziara yake kilichofanyika mkoani Mtwara.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt.Biteko amewataka viongozi mbalimbali kuona kuwa malalamiko yaliyotolewa na Wananchi wakati wa ziara yake yakiwemo ya umeme, maji na gawio la ushuru wa huduma ni ya haki na hivyo wajibu wa viongozi hao ni kutatua matatizo ya wananchi.
“Nikianzia Songosongo ambapo Gesi inatoka, wananchi pale wana malalamiko yote ya msingi, mfano kuna watu walikuwa wakifanya kazi za ulinzi katika mitambo na visima vya Gesi, pesa yao hawajalipwa kwa miaka kadhaa sasa, hivyo, madai haya TPDC na Songas mtayalipa, Serikali ya Awamu ya Sita hataivumilia kuona jambo hili linafanyika, TPDC hakikisha ndani ya mwezi wa Disemba, hawa watu wote wawe wamelipwa pesa zao,” amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa, katika Kisiwa cha Songosongo kuna uwanja wa Ndege unaohudumia ndege zinazowabeba viongozi, watendaji na wataalam mbalimbali huku wananchi wakiwa hawana usafiri wa uhakika utakaowatoa kisiwani kwenda Kilwa kwenye Makao Makuu ya Wilaya, hivyo, ameiagiza TPDC kwa kushirikiana na kampuni ya PAN AFRICAN ENERGY na SONGAS kutafuta kivuko na kukipeleka kwenye kisiwa hicho ili kiwasaidie wananchi.
Kuhusu kero ya upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Kisiwa cha Songosongo, Dkt. Biteko ameagiza kuwa, umeme unaoendesha mitambo ya TPDC na PAN AFRICAN ENERGY uende pia kwa wananchi wa Kisiwa hicho na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) uende Songosongo tarehe 18 mwezi huu ili kuanza hatua za kusambaza umeme kwa wananchi wapatao takriban 5000.
Akizungumzia malalamiko ya Wananchi katika kijiji cha Msimbati na Madimba wilayani Mtwara kuhusu kituo cha Afya, Dkt. Biteko ameagiza TPDC kujenga kituo cha Afya kizuri na cha kisasa katika moja ya Vijiji hivyo ili wananchi wafaidi matunda ya kuwepo kwa mradi wa Gesi Asilia ambao pia wao wamekuwa walinzi.
Aidha, ameagiza TPDC kukarabati kituo cha Polisi na kuweka taa za barabarani ndani ya Mwezi wa 12 na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuendelea kusambaza umeme kwenye Vijiji hivyo ambapo ameagiza umeme huo utoke Mnazi Bay na katika Mitambo ya Madimba ili wananchi hao wapate umeme wa uhakika.
Kuhusu suala la ushuru wa huduma ambao kijiji cha Songosongo kinaidai Halmashauri ya Kilwa kutokana na makubaliano ya awali ya kupewa asilimia 20 ya gawio ambazo hawakupewa kwa muda mrefu na kupelekea fedha hizo kufikia milioni 400, ameagiza uongozi wa Mkoa wa Lindi kuhakikisha kuwa fedha hizo zinarudi katika Kijiji cha Songosongo.
Kuhusu ushuru wa huduma kwa Vijiji vya Msimbati na Madimba mkoani Mtwara, ambapo Halmashauri ya Mtwara inapata shilingi Bilioni 1 na Milioni 500 kutoka TPDC na kampuni ya Maurel & Prom, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara kuhakikisha sehemu ya hizo fedha zinarudi katika Vijiji hivyo ili wananchi waone tofauti ya uwepo wa miradi kwenye maeneo yao na kuendelea kuunga mkono miradi ya Serikali.
Vilevile, kuhusu hali ya kukatika kwa umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, Dkt.Biteko amewataka TANESCO kuja na suluhisho la changamoto hiyo kwani mikoa hiyo kwa sasa inahitaji megawati 22 na kwamba inajengwa njia ya kusafirisha kutoka Songea-Masasi hadi Mahumbika ambayo itasaidia mikoa hiyo kupata pia umeme wa Gridi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kutojificha kwenye kichaka cha taratibu za manunuzi ambacho kimepelekea mtambo mmoja wa umeme mkoani Mtwara kutofanya kazi kwa miaka miwili na kuongeza
kuwa Serikali inaiangalia menejimenti ya TANESCO lakini kwa sasa ijitathmini na ijikite kwenye kupelekea watu umeme na wawe kimbilio la wananchi.
Aidha, ameitaka TANESCO Makao Makuu kutojilundikia majukumu ikiwemo ya manunuzi ambayo yanarudisha nyuma shughuli za shirika na kuleta urasimu.
Pamoja na kuipongeza TPDC kwa majukumu inayofanya, ameitaka kuja na mpango wa muda mrefu wa upatikanaji wa Gesi Asilia na Mafuta nchini hali itakayoihakikishia nchi uhakika wa uwepo wa nishati hiyo ambayo matumizi yake duniani yanazidi kuongezeka.