Kikosi cha Simba Queens kimeweka wazi kuwa, kinafanya mazoezi makali kujiweka fiti kwa mashindano ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara msimu ujao yanayotarajiwa kuanza Desemba 15, mwaka huu.
Kabla ya ligi hiyo kuanza, msimu mpya utafunguliwa kwa michezo wa Ngao ya Jamii itakayoanza Desemba 8, mwaka huu ikishirikisha timu za Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess na Fountain Gate Princess.
Meneja Simba Queens, Selemani Makanya, amesema kocha wa kikosi hicho, Mussa Mgosi anawaandaa vyema wachezaji wake ili kuwa na msimu bora.
Makanya amesema lengo la kocha huyo ni kuiongoza timu yake kufanya vyema katika msimu ujao na kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ambao msimu uliopitwa ulibebwa na JKT Queens.
Amesema kikosi hicho kilianza mazoezi Novemba 7, mwaka huu na kocha Mgosi amekuwa akikiandaa vizuri kufanya makubwa.
“Tumeanza kambi mapema ili kujiandaa kwa msimu mpya kwani hatutaki kuona msimu ujao tunapoteza tena ubingwa, tunaamini kwa asilimia 100 taji litarajea mikononi mwetu,” amesema.
Katika nyakati nyingine, timu imetangaza kumnasa nyota Isabelle Diakiese kutoka Bikira FC ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).