Imefahamika kuwa Uongozi wa Simba SC  unaendelea kukuna vichwa kufuatia kusaliwa na majina matatu ya Makocha walioomba kazi klabuni hapo, baada ya kuondoka kwa Kocha Robert Oliviera ‘Robertinho’ juma lililopita.

Hadi sasa makocha wanaotajwa kusalia katika kinyang’anyiro hicho ni Mtunisia Nasreddine Nabi aliyekuwa Young Africans msimu uliopita, Mbeligiji Sven Vandenbroeck aliyewahi kuinoa timu hiyo na Mualgeria Abdelhak Benchikha aliyetwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akiwa na USM Alger akiinyang’anya Young Africans tonge mdomoni.

Taarifa zinaeleza kuwa, kati ya makocha watatu hao, mtu ambaye Simba SC inaweza kumpata kwa uharaka na rahisi ni Benchikha kuliko ilivyo kwa Sven na Nabi.

Sven ni miongoni mwa makocha walioingia tatu bora ya waalimu wanaotakiwa, lakini kuna baadhi ya viongozi wamemkataa kutokana na misamamo yake huku wengine waliwahi kukwaruzana naye kipindi yupo kikosini hapo kuanzia Disemba 2019 hadi Januari 2021, wanaamini akirejea hawataelewana vyema.

Kwa upande wa Nabi, Simba SC ni kama imevuta pumzi na kuamua kuachana naye kutokana na kile kinachoelezwa kocha huyo anahitaji vitu vingi ikiweno kupunguza wachezaji karibu wote kikosini.

Benchikha mwenye uzoefu wa kutosha na soka la Afrika akifundisha tangu mwaka 2001, mara nyingi ameonekana kuwa kocha mwenye asili ya kujilinda na kutumia mfumo wa mabeki wanne, viungo wa chini wawili, wajuu wa tatu na mshambuliaji mmoja (4-2-3-1) kama ilivyokuwa kwa Robertinho jambo linalowapa kigugumizi baadhi ya wafanya maamuzi wa Simba SC.

Hata hivyo pamoja vigogo wa Simba SC kutopitisha moja kwa moja jina la Benchikha, na kuamua kupitia wasifu wa makocha wengine lakini Muargeria huyo bado ana nafasi kubwa ya kupewa kibarua kuliko ilivyo kwa Nabi na Sven ambao walitajwa hapo awali.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally alisema harakati za kumpata kocha mpya zinaendelea na atatangazwa siku si nyingi.

“Tutaleta kocha anayefaa kuifundisha Simba SC, tuna majina tayari na tunaendelea na mchakato wa kuchambua na kuamua nani tumpe timu yetu kutokana na matakwa yetu na tutawatangazia,” alisema Ahmed huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Imani Kajula akijibu kwa ufupi akisema; “Tupo katika hatua za mwisho kumpata kocha mpya.”

Simba SC kwa sasa ipo chini ya kocha wa makipa Mhispanyola Dani Cadena ambaye pia ana sifa zote za kuwa kocha mkuu, akisaidiana na nguli wa timu hiyo, Seleman Matola wakiendelea na maandalizi ya mechi ijayo, hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas Novemba 25, kwa Mkapa.

KMC kukipiga na mabingwa wa Sudan
RC Sendiga aagiza kazi saa 24 miradi ya Barabara