Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi ahakikishe wafugaji wote walioingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha uharibifu wa mazao na wananchi kukosa chakula wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwani hakuna yeyote aliye juu ya sheria wananchi wote ni sawa.

Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi kwenye vijiji vya Namkatila, Matambarale na Nandandala akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Vijiji hivyo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo mkulima mmoja aliuawa.

Amesema, “Serikali iko macho na itamchukulia hatua yeyote anayeathiri shughuli za wengine, Tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, hivyo watendaji wote wa vijiji wawajibike kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuepusha migogoro isiyokuwa na tija. Tutaendelea kuwalinda wananchi. Ukifuata utaratibu hakuna shida, tufuate sheria.”

Aidha, Majaliwa ameongeza kuwa Serikali haitovumilia kuona jamii ya wafugaji wasiozingatia sheria na haitotoa nafasi kwa wakulima kuendelea kuharibiwa mazao yao. “Jambo hili halikubaliki na hatua kali zitachukuliwa kwa watu wote wanaotaka kuvuruga amani, Serikali haitovumilia vitendo hivyo.”

“Hatutamsamehe mfugaji anayetumia fimbo yake kumpiga mkulima baada ya kulisha mifugo kwenye shamba lake. Hatuna nafasi ya kushuhudia hayo, utaratibu lazima uzingatiwe, lazima tukomeshe migogoro ya wafugaji na wakulima. Tumuache mkulima aendelee kulima avune. Tusilinde waovu,” ameongeza Waziri Mkuu.

Young Africans wavamia Algeria kimya kimya
Watoto watano wafariki kwa kula Chakula chenye sumu