Scolastica Msewa, Mkuranga – Pwani.

Mwenyekiti wa Chama kikuu Cha Ushirika wa Wakulima wa Mkoa wa Pwani – CORECU, Musa Mngeresa amewataka Wakulima mkoani humo kuendelea kulinda ubora wa korosho zao kwa kuokota Korosho kila siku ili zibaki kwenye ubora stahiki hasa ni kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha nchini kote.

Akihutubia katika mnada wa pili wa Korosho ulifanyika katika Ghala kuu la Wilaya ya Mkuranga Kijiji cha Kingoma, Mngeresa amesema Korosho zikidondoka mtini isilale shambani haraka ziokotwe ikahifadhiwe vizuri ili kulinda ubora wake.

Amesema, “Korosho ikidondoka haitakiwi kulala ardhini na iwapo italala shambani hapo bila kuokotwa itaingiwa na unyevu ambao hupelekea kupunguza ubora wa korosho ya mkulima hivyo tuokote Korosho zetu mara kwa mara.

Akizungumzia maandalizi ya kilimo cha zao la mbaazi ambalo ni zao jipya la biashara mkoani humo Mngeresa amesema tayari wamenunua Tani 3 za mbegu za mbaazi ambazo zipo hatua za mwisho za ugawaji kwa Wakulima.

Akitoa taarifa kwenye mnada wa pili uliofanyika November 15, 2023 Meneja wa Chama kikuu Cha Ushirika wa Wakulima wa Mkoa wa Pwani – CORECU Mantawela Hamisi alisema Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimeathiri uuzaji wa zao la Korosho mkoani Pwani ambapo Tani zaidi ya 1500 zilishindwa kuuzwa katika mnada wa pili wa November 8 mwaka huu kutokana zao hilo kuingiwa na unyevu ambao ni hatari kwa zao hilo.

Amesema Korosho hizo Tani zaidi ya 1500 zimeunganishwa kwenye Tani 3187 zilizouzwa kwenye mnada huu ambapo bei ya wastani wa shilingi 1809.46 kwa kilo moja na kwamba athari ya mvua ni kubwa lakini lengo la mkoa wa Pwani ni kuuza Korosho zenye ubora hivyo tunahimiza Wakulima kuendelea kuanika Korosho zao kila jua linapowaka hadi zitakapokauka.

“Wakulima bado wana Korosho nyingi majumbani wakiendelea kukausha kuondoa unyevu hivyo zinavyokauka watapeleka kwenye vyama vya msingi ili zipelekwa kwenye maghala ya Chama kikuu CORECU tayari kwa kuuzwa,” alisema.

Kwa upande wake Mkulima wa korosho, Sultani Juma ameshukuru kwa ajili ya bei nzuri ya Korosho katika minada hiyo ukilinganisha na hali ya hewa ya mvua na kusema mvua zimekuwa nyingi hivyo uwezo wa kuzihifadhi na kuzikausha ni kazi ngumu.

Ahmed Ally: Tuzo ya AFL haitakaa ofisini
Wachezaji Simba SC waombwa kupambana