Mkuu wa Ushirikishaji jamii Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hamis Mngwana amewataka Viongozi na Wamiliki wa Kampuni Binafsi za Ulinzi kuhakikisha wanashirikiana na Jeshi la Polisi, ili changamoto zinazowakabili ziweze kutatuliwa.
Mngwana ameyasema hayo katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika jengo la Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ambapo amewataka kuunda umoja wao utakao waunganisha katika shughuli zao za ulinzi badala ya kila kampuni kufanya kazi kivyake.
Amesema, “nia ya kamisheni hii ya Ushirikishwaji jamii ni kuwa na mahusiano mazuri baina ya wananchi na jeshi la Polisi, lakini pia tutafanikiwa kuzuia uhalifu kama tutashirikia kwa pamoja katika kubaini, kutanzua na kuzuia uhalifu katika maeneo yetu.”
Kwa upande wake Meneja wa tawi la Kampuni Binafsi ya Ulinzi Salu Security, Kalebi Samson Munkenyi amemuomba Mkuu huyo kushughulia changamoto ya kukamatwa na Polisi pale tatizo linapotokea malindoni bila kuacha mlinzi katika maeneo hayo jambo ambalo linawasababishia hasara mara mbili.