Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amelitaka Jeshi la Polisi nchini kutenda haki wakati wote wa utendaji wao wa kazi, wachukie rushwa na wajikite katika kutatua matatizo ya watanzania kwani usalama wa watanzania upo mikononi mwa Jeshi hilo.

Amesema hayo Novemba 16, 2023 wakati wa kilele cha mahafali ya kufunga mafunzo Namba 1/2022/2023 ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi Tanzania iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi jijini Dar es Salaam.

Tendeni haki, kwani haki hulistawisha
Taifa, anayestahili haki apate na anayestahili adhabu apate, anayestahili kwenda mahakamani aende kwa haki, msibambikie watu kesi pia chukieni rushwa kwani rushwa hupofusha akili ya Binadamu,” Amesisitiza Dkt.Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amelitaka Jeshi la Polisi kutoona fahari ya vyeo wanavyopata, bali fahari ya kazi itokane na huduma wanayotoa kwa watanzania hivyo wajikite kwenye kusikiliza mahitaji ya wananchi kwani wananchi wanachohitaji ni uwepo wa Jeshi la Polisi imara litakalohakikisha usalama wao.

Kuhusu ujenzi wa majengo ya Utawala katika Chuo hicho ambayo bado hayajakamilika, ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani isimamie utekelezaji wa suala hilo kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi majengo katika Chuo hicho.

Vilevile, ametaka Polisi wote Tanzania kulipa heshima Jeshi la Polisi na atakayetokea kuharibu heshima ya Jeshi hilo, ashughulikiwe. Amewataka pia washirikishane na kuwa na umoja huku wakitambua kuwa Jeshi la Polisi ni duru ya amani ya nchi.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, IGP Camillus Mongoso Wambura, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi waliomaliza kozi hiyo walisoma kwa muda miezi Tisa na na wanafunzi 952 wametunukiwa vyeo ambapo mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na kuimarisha weledi na umakini katika maeneo ya kazi.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Novemba 17, 2023
Majanga yamuondoa Dalot kikosi cha Ureno