Wakala wa Nishaji Vijijini – REA, umeanza utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wa kuwafikishia huduma ya umeme wakazi wa Madimba na Msimbati kwa kufanya tathmini katika maeneo hayo ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu alifanya ziara ya tathimini katika kata za Madimba na Msimbati, ili kuona hali halisi kabla ya kuanza utekelezaji.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Madiwani wa Kata za Msimbati na Madimba, Balozi Meja Jenerali Kingu amesema REA itahakikisha maelekezo hayo yanatekelezwa ambapo Novemba 18, 2023 watakutana na mkandarasi kwa ajili ya kujadili ujenzi wa miundombinu ya umeme katika kata hizo.

Amesema, “tutahakikisha utekelezaji wa haraka unafanyika na wataalamu wanapita ili kuona hali halisi na uhitaji katika maeneo husika, hivyo Wananchi wa maeneo haya watoe ushirikiano wataalamu wa REA na mkandarasi ili kuharakisha uratibu wa kazi hiyo.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu (wa pili kushoto), akijadiliana jambo na Diwani wa Kata ya Msimbati Rashid Linkoni (wa pili kulia) na Viongozi wengine kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Mwenyekiti na Ujumbe wake walifika eneo hilo Novemba 16, 2023 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko ya kufikisha umeme Msimbati na Madimba.

Aidha, ameongeza kuwa Bodi na Menejimenti ya REA watafuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri Mkuu la kuyafikishia maeneo hayo umeme huku akitaka taarifa zitolewe haraka endapo kutakuwa na changamoto katika utekelezaji wa mradi huo ili zipatiwe ufumbuzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Vijijini, Mhandisi Jones Olotu aliwahakikishia Maafisa Watendaji wa Kata hizo mbili kuwa wiki ijayo wakandarasi watafika kukutana nao kwa ajili ya kuoneshwa maeneo na vijiji vinavyotakiwa kufikishiwa umeme huku Diwani wa Kata ya Msimbati, Rashid Linkon akiishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuhakikisha wanapata umeme na kunufaika na rasilimali ya gesi asilia inayopatikana eneo hilo.

Naye Diwani wa Kata ya Madimba, Idrisa Kujebweja, alitoa pongezi kwa mwitikio wa haraka ambao umeoneshwa na REA katika kufanyia kazi maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na kuahidi kwamba, watatoa ushirikiano wote utakaohitajika.

Dkt. Biteko, akiwa katika ziara ya kazi mkoani Mtwara hivi karibuni aliitaka REA kuangalia ni namna gani inaweza kuwaunganishia umeme wananchi wa maeneo hayo na kujenga miundombinu ili waweze kunufaika na nishati ya gesi asilia inayozalishwa katika eneo hilo.

Polisi wazima jaribio la wizi, wawili wajeruhiwa
Watoto Njiti wapewa upendo nyanja za Elimu, Afya