Takriban Vijana wapatao 37 wamefariki dunia, kufuatia mkanyagano uliotokea usiku wa kuamkia Novemba 20, 2023 wakati wa zoezi la kuwasajili makuruta wa kijeshi katika mji Mkuu wa Jamhuri ya Congo, Brazzaville.
Waziri Mkuu wa Taifa hilo, Anatole Collinet Makosso amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema licha ya vifo hivyo pia kuna idadi ya watu ambayo bado haijajulikana waliojeruhiwa katika uwanja wa Michel – Ornano.
Wiki iliyopita, Jeshi katika taifa hilo la Afrika ya kati pia linalojulikana kama Congo-Brazzaville, lilitangaza kuwa linaajiri watu 1,500 wenye umri wa kati ya miaka 18 na 25 ambapo wengi walijitokeza.
Hata hivyo, chanzo cha mkasa huo bado hakijabainika wazi, lakini mashuhuda wamesema baadhi ya watu walikuwa wakijaribu kuingia kwa nguvu uwanjani hapo, jambo lililosababisha mkanyakagano.