Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi, George Katabazi amewataka Maafisa na wakaguzi waliohitimu mafunzo yao katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), kuzingatia haki na weledi katika utendaji wao ili kuepuka malalamiko katika Jamii.
Katabazi ameyasema hayo wakati akizungumza na Maafisa na Wakaguzi hao, mara baada ya kuripoti ofisini kwake tayari kwa kuanza majukumu na kuwataka vyeo walivyovipata wavitendee haki kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria na kutoa elimu ya ushirikishaji jamii, ili kuzuia uhalifu na wahalifu.
Amesema, Wakaguzi watakaopangiwa Kata wawe wabunifu kwa kujenga mahusiano ya karibu na jamii ili kupata taarifa za wahalifu na uhalifu na kuzifanyia kazi na kwamba Jeshi la Polisi lina wajibu wa kulinda raia na mali zao hivyo ni jukumu la maafisa na wakaguzi hao kuhakikisha wahalifu na uhalifu unadhibitiwa bila kumuonea mtu.
Maafisa na Wakaguzi hao wahitimu, wanatarajia kuongeza chachu katika utendajj wa Jeshi Hilo kwa kusimamia kauli mbiu ya Nidhamu, Haki na Weledi kama msingi wao wa mafanikio.