Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya uwepo mvua kubwa kwa muda wa siku tano kwenye maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia pamoja na Visiwa vya Pemba na Unguja kuanzia Novemba 21-25, 2023.
TMA imetoa angalizo kwa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, ambapo athari zinazoweza kujitokeza ni Mafuriko kuathiri maeneo machache, athari kwa usafirishaji, baadhi ya barabara kutopitika na vifo vinaweza kujitokeza kutokana na mafuriko pamoja na kuathirika kwa baadhi ya Shughuli za Kiuchumi.
Itakumbukwa Agost 26 TMA ilitoa taarifa ya ya uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa za el nino ambazo huenda zikasababisha vifo, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu kuanzia oktoba hadi disemba 2023.
Aidha TMA ilisema mvua hizo zitasababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, upotevu wa mali na madhara kwa binadamu na mazingira.
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a alisema utabili unaonyesha mvua zitakuwa juu ya wastani huku akisahuri sekta mbalimbali zijiandae kukabiliana na majanga.
”Mvua za vuli zinatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu katika maeneo mengi nchini na zitakuwa na wastani na wastani wa juu itanyesha Pwani ya kaskazini na Ukanda wa ziwa victoria” alisema Chang’a.
Maeneo mengine ni Magharibi mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa kigoma wilaya ya kakonko na kobondo, ukanda wa Pwani ya Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro , Pwani ,Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba