Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP. Richard Thadei Mchomvu amewataka Wakaguzi wanaohudumu katika shehia kuunda makundi ya Whatsapp wakijumuisha wananchi wa maeneo ya shehia zao, ili kurahisisha kupata taarifa za matukio kwa haraka.

Kamanda Mchomvu ametoa kauli hiyo wakati alipofanya kikao na Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa shehia zilizopo ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kuongeza kuwa Wakaguzi shehia ni watendaji muhimu katika ngazi ya shehia hivyo kuunda makundi hayo kutarahisisha upatikanaji wa taarifa katika shehia zitakazosaidia kuzuia uhalifu.

Amesema, “unapounda magroup ya Whatsapp inasaidia kuwa na shehia yako kiganjani kwa maana muda wote inakuwa rahisi kujua jambo lolote linaloendelea katika eneo lako hata ikiwa hauko eneo hilo kwa muda huo.”

Hata hivyo, aliwataka kuendelea kufanya kazi kwa kutenda haki na uadilifu kwani ndio nguzo katika utekelezaji wa majukumu ndani ya Jeshi la Polisi kwa kuwa haki na uadilifu huwajengea imani wananchi kwa Jeshi lao.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Cleaophance Alphonce Magesa aliwapongeza wakaguzi hao kwa kufanya kazi kwa bidii katika shehia zao na kuwasisitiza kuwa wabunifu wa kuboresha utekelezaji wa majukumu ili kuendelea kujenga taswira njema ndani ya Jeshi la Polisi.

TAWA kushughulikia tatizo uvamizi wa Tembo uraiani
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Novemba 24, 2023