Kocha Mkuu wa Simba SC Abdelhak Benchikha amechimba mikwara kwa kuwataka mastaa wote wa kikosi chake kuwa tayari kwa maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Gwaneng Galaxy ya Botswana.
Benchikha anatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo Jumatatu (Novemba 27), kuchukuwa nafasi ya Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinhơ’ aliyefutwa kazi baada ya kichapo cha 5-1 ilichopata timu hiyo mbele ya Young Africans.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria alitangazwa Ijumaa (Novemba 24) majira ya usiku, na rasmi alianza safari ya kuelekea Dar es salaam, Tanzania saa 24 baadae.
Akiwa njiani kuelekea Dar es salaam, kocha huyo amesema kitu cha kwanza anataka kuwaona wachezaji wote kisha ataanza kusuka mipango yake kuelekea mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Naijua Simba SC ni timu nzuri na imekuwa na ushindani mkubwa katika bara hili la Afrika, nina furaha kujiunga nao. Kwa sasa siwezi kusema chochote kuhusu mipango yangu binafsi, naenda kutimiza mipango ya timu kutokana na makubaliano yetu,” amesema Benchikha
“Kitu cha kwanza nitakachofanya ni kukutana na wachezaji wote kambini, nataka nionane na kila mmoja na kutambua uwezo wake na baada ya hapo nitaanza kutengeneza timu nikiendeleza nilipoikuta.”
Pia kocha huyo aliyetwaa mataji nane hadi sasa ikiwemo CAF Super Cup alilobeba mara mbili na Kombe la Shirikisho Afrika alilotwaa msimu uliopita akiwa na USM Algers akiitibulia Young Africans kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 amesema anajua kiu ya Simba ni kufanya vizuri zaidi kimataifa na anauzoefu na michuano hiyo hivyo yupo tayari kwa vita.
“Mashindano ya kimataifa ndio shauku kubwa ya timu nyingi Afrika ikiwemo Simba SC. Kwa bahati nzuri nimekuwa kwa muda mrefu kwenye soka la Afrika nalijua vizuri na nimefanya kazi kwa mafanikio barani hapa, nipo tayari kushirikiana na Simba kuanzia viongozi, benchi la ufundi na wachezaji kuhakikisha nafika malengo,” amesema Benchikha.
Benchikha ataanza kuiongoza Simba SC kwenye mechi ya michuano ya CAF, itakayopigwa Desemba 2 ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ukiwa ni mchezo wa pili kwenye Kundi B.