Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’ amefunguka kuwa, kwa sasa wanakwenda kwenye ukurasa mpya na klabu hiyo.

Jumapili (Novemba 26), Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC pamoja na wachezaji wa timu hiyo, walifanya kikao cha takribani siku nzima, lengo likiwa ni kufahamu changamoto zilizopo ambazo huenda zinasababisha wapitie kwenye kipindi kigumu kwa sasa.

Kikao hicho kiliongozwa na Try Again na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kikao hicho, muafaka umepatikana wa kuyafikia malengo yao waliyoyalenga msimu huu 2023/24.

Kwenye kikao hicho, Wachezaji wa Simba SC waliahidi kuipambania nembo ya klabu hiyo, pamoja na kuyafikia malengo ambayo ni kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sambamba na kurejesha furaha kwa Mashabiki wao.

Kikao hicho kimeamua kutengeneza ukurasa mpya baada ya magumu ambayo wamepitia Simba SC ndani ya michezo mitatu iliyopita.

Ikiwemo kula chuma 5-1 mbele ya Young Africans, sare ya 1-1 na Namungo FC, kisha sare ya 1-1 na ASEC Mimosas kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya kikao hicho, Try Again aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram akisema: “Ukurasa Mpya.”

Moja ya Wajumbe wa Bodi ya Simba ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alisema: “Kauli ya mwenyekiti wetu ina maana kubwa sana, sasa tunakwenda kufanya makubwa na timu yetu imefungua ukurasa mpya wa kuyafikia malengo yetu.”

Tayari Kocha Mkuu wa Simba SC Abdelhak Benchikha amewasili nchini sambamba na wasaidizi wake Kamal na Farid na wanatarajiwa kuanza kazi leo kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy.  

Nunez kuichomoa pesa Liverpool
Wanawake watakiwa kuwa imara kuokoa familia