Kiungo kutoka nchini Ubelgiji Kevin de Bruyne amethibitisha kuwa anatarajia kurejea katika kikois cha Manchester City mapema mwaka 2024, huku akiwa mbioni kupona kwake kutokana na jeraha la misuli ya paja.
Kiungo huyo alipata tatizo baya la misuli ya paja katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita na alicheza kwa dakika 49 tu mwanzoni mwa msimu huu, kabla ya kupata jeraha lingine ambalo hatimaye lilihitaji upasuaji.
Mapema mwezi huu, De Bruyne alilinganisha misuli yake ya paja na “taulo ya jikoni iliyolowa” huku akikiri ukubwa wa uharibifu uliopatikana, lakini alikiri kuwa hajui tarehe ya kurudi dimbani.
Kwa kuwa sasa amefanyiwa uchunguzi huo, De Bruyne aliiambia Sky Sports F1 alipokuwa mgeni kwenye mashindano ya Grand Prix ya Abu Dhabi yanayoisha msimu huu kwamba atarejea dimbani mapema 2024.
“Naendelea vizuri,” alisema juu ya kupona kwake. Bado tuna njia ndogo ya kwenda, lakini tutafika.”
Alipoulizwa tarehe anayoweza kurejea, De Bruyne aliongeza: “Tunatumaini kuwa kuna kitu karibu baada ya mwaka mpya, ikiwa kila kitu kitaenda sawa.”
City watamaliza kampeni zao za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya Desemba kwa michezo dhidi ya RB Leipzig na Crvena zvezda, huku kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola pia kikiwa na mechi sita za Ligi Kuu England kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Tottenham Hotspur ndio wapinzani wanaofuata kwenye ratiba ya nyumbani, wakifuata Aston Villa, na De Bruyne ni wazi hataweza kuwakabili.
De Bruyne pia atakosa kampeni ya kwanza ya City Klabu Bingwa Dunia ya FIFA, ambayo inatazamiwa kuanza Desemba 19, mwaka huu kwa mechi ya Nusu Fainali dhidi ya Leon ya Mexico au Urawa Red Diamonds ya Japan.
Mchezo wa mchujo wa mwisho na wa mshindi wa tatu utafanyika Desemba 22, mwaka huu nchini Saudi Arabia, siku tano tu kabla ya City kurejea England kucheza na Everton.