Eva Godwin – Dodoma
Chama cha Mapinduzi – CCM, Mkoa wa Dodoma kimemuagiza Afisa Biashara na mamlaka zinazohusika, kusitisha kuwaondoa Mawakala usafirishaji abiria waliopo eneo la Makole jirani na Chuo cha Biashara – CBE, jijina Dodoma.
Agizo hilo, limetolewa na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Jawadu Mohammed hii leo Novemba 29, 2023 alipowatembelea Mawakala hao baada ya kupokea malalamiko ya kufukuzwa na kufungiwa vibanda vyao vya kufanya shughuli hizo Jijini Dodoma.
“Nchi hii inaendeshwa kwa taratibu,Sheria na desturi kwahiyo lazima katika maeneo mengine Jiji na mamlaka zinazohusika zisiwe na mkono waharaka wakufunga biashara za watu,” amesema.
Jawadu ameongeza kuwa, wakati chama kikitoa agizo hilo, pia wahusika wanatakiwa kuhakikisha Mabasi hayapakii wala kushusha abiria katika eneo hilo na badala yake yafanye hivyo katika vituo husika.
Hata hivyo, amewataka mawakala hao kutii sheria, taratibu na miongozo ya nchi na kusema “ndugu zangu nataka niwaelezee juu ya kutii sheria, taratibu na miongozo ya Nchi, utii huu unatufanya sisi kuwa salama katika kazi hizi tunazozifanya, lakini la pili kutotumia muda mwingi kuhangaika na masuala ya kesi na mivutano nakukimbizana na migambo.“
Aidha, Jawadu ameongeza kuwa, “CCM Mkoa wa Dodoma tutahakikisha tunakuwa sauti yenu, lakini tutaendelea kusimamia ustawi wa Mji wa Dodoma kwa kuhakikisha wananchi ambao ni wapiga kura wetu hawarudishwi nyuma kwenye maendeleo yao ya utafutaji wa kipato.”