Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi ametamba na kusema wachezaji wake hawaiogopi Al Ahly na wapo tayari kupambana nayo kupata ushindi.
Gamondi amesema hayo, kuelekea pambano la Mzunguuko wa Pili wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam saa moja jioni.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanashinda mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
“Wachezaji wangu wanatambua umuhimu wa mechi za Ligi ya Mabingwa na kitu ambacho kinatakiwa ni pointi tatu, hivyo watapambana kufanya vizuri na kuwapa burudani mashabiki, baada ya kukosa matokeo katika mchezo wa kwanza wa michuano hii,” amesema.
Young Africans itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwa mabao 3-0 katika Mchezo wa mzunguuko wa Kwanza wa Kundi D dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.
Gamondi amesema hawataingia kwa kuwaogopa wapinzani wao bali wataingia kwa kuwaheshimu katika mchezo huo.
Hata hivyo, Meneja Habari wa klabu ya Young Africans, Ali Kamwe amewaita mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kujaa kwa wingi uwanjani ili kujionea burudani kutoka kwa wachezaji wao.
“Hatuna tunachokiogopa kwani tuna wachezaji wazuri na walimu wenye viwango hivyo tunahitaji sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wetu ili kuweza kuwaongezea hamasa wachezaji wetu waweze kufanya vizuri,” amesema Kamwe.