Mshambuliaji kutoka nchini Argentina Lautaro Martinez yuko tayari kusaini mkataba mpya na Inter Milan licha ya kutakiwa na klabu za Chelsea na Manchester United.
Mkataba wa sasa wa Nahodha huyo wa Inter Milan, unatarajiwa kumalizika ifikapo 2026, na wawakilishi wake wamefanya mazungumzo na Chelsea na Manchester United katika miezi 18 iliyopita kabla ya uwezekano wa kuhama kutoka Italia kwenda England.
Taarifa zinaeleza kuwa mwezi Juni, mwaka huu klabu mbili za Ligi Kuu England pamoja na Real Madrid, zote zilionyesha nia ya kumsajili Mshambuliaji huyo wa Argentina.
Licha ya hayo, Inter waliendelea kumshikilia nyota wao wakati wa dirisha la Usajili, na tangu wakati huo wamekuwa na nia kubwa ya kumsainisha mshambuliaji huyo kwa mkataba wa muda mrefu katika klabu hiyo, kabla ya majira ya joto ya 2024.
Martinez kwa sasa yuko tayari kusaini nyongeza ya mkataba na Nerazzurri baada ya kuwa na mwanzo bora kwa msimu wa 2023/24.
Nyota huyo amekuwa katika kiwango cha hali ya juu, akifunga mabao 13 katika mechi 13 za Serie A msimu huu, likiwamo bao muhimu la kusawazisha katika mchezo wa Jumapili (Novemba 26) wa dabi ya Italia dhidi ya wapinzani wao wakuu, Juventus kwenye Uwanja wa Allianz.
Kiwango cha nahodha huyo kimeifanya Inter kukaa kileleni mwa msimamo wa Serie A, pointi mbili mbele ya wapinzani wao wa karibu Juve, na pia kushinda mara tatu na sare katika mechi zao nne za kwanza za makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.