Afisa Habari wa Mabingwa wa Soka Tanzania bara Young Africans Ally Kamwe amesema kuwa watautumia mchezo dhidi ya wapinzani wao Al Ahly ya nchini Misri kama daraja la kuitafuta historia ya kuwa klabu namba moja Barani Afrika.
Hiyo ni katika kuelekea Mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utakaopigwa kesho Jumamosi (Desemba 02), Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa moja usiku
Young Africans itaingia uwanjani kuvaana dhidi ya Al Ahly, wakiwa na hasira za kutoka kufungwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad ya nchini Algeria, katika Mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Kundi D.
Kamwe amesema kuwa wanataka kuutumia mchezo huo mkubwa dhidi ya Al Ahly, kupanda katika viwango vya ubora vya soka Barani Afrika kwa kuwafunga kuanzia nyumbani kabla ya kwenda kurudiana kwao Misri.
Kamwe amesema anaamini ubora wa wachezaji wao ambao wamewasajili katika msimu huu, baadhi ni Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Koussi Yao ambao wana uzoefu mkubwa wa kucheza michuano hiyo ya kimataifa.
Ameongeza kuwa malengo hayo yatatimia kama mashabiki watajitokeza uwanjani kuujaza Uwanja wa Mkapa, kuwasapoti wachezaji watakaokuwepo wakiipanmbania timu yao.
“Tunakwenda kucheza na timu namba moja kwa ubora Barani Afrika, hilo lipo wazi kabisa kila mtu anafahamu ubora wa Al Ahly, lakini sisi pia tupo namba tano kwa ubora hivyo mchezo huo hautakuwa rahisi.!
“Kwetu kama uongozi na wachezaji, tunafurahia kukutana na timu hiyo, bora Barani Afrika kwani ili uwe bora lazima ukutane na timu bora na kuifunga.
“Tukimfunga huyo Al Ahly ambaye namba moja, hiyo itatufanya tupande viwango vya ubora vya soka Afrika, na hilo Ilinawezekana kwetu kutokana na ubora wa kikosi chetu,” amesema Kamwe.