Kamati ya Mashindano ya Klabu ya Young Africans imeweka mpango mkakati wa kuipeleka klabu hiyo Hatua ya Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa kuwaongezea Bonasi Wachezaji katika mchezo wao wa kesho dhidi ya AI Ahly.
Young Africans ambao wanaburuza mkia kwenye Msimamo wa Kundi D, kufuatia kuanza vibaya kwą kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria, kesho Jumamosi (Desemba 02) wanatarajiwa kuwakaribisha Mabingwa watetezi Al Ahly kwenye kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam kuanzia saa moja usiku.
Ikumbukwe kuwa mabosi wa Young Africans katika hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo waliwaondoa Al Merrikh ya nchini Sudan na ASAS ya Djibout, mabosi hao waliweka Bonasi ya Sh Milioni 250 kwa ajili ya Wachezaji na Benchi la Ufundi la timu hiyo kwa kila mchezo.
Mmoja wa Mabosi wa Young Africans, amesema wanataka kuona hamasa na morali ya wachezaji inaongezeka, hivyo wamepanga kuwaongezea Bonasi wachezaji wao ili malengo yafanikiwe msimu huu.
Bosi huyo amesema kuwa Bonasi hiyo huenda ikafikia Sh. Milioni 300 hadi 350m.
“Mara baada ya kupoteza mchezo wetu wa kwanza wa hatua ya makundi mbele ya Belouizdad, ni lazima tuhakikishe tunapata matokeo katika mchezo huu wa pili ambao ni muhimu sana kwetu ili kurejesha matumaini ya kucheza Robo Fainali.
“Hivyo basi uongozi umepanga kuongeza bonasi katika mechi hii kikubwa tunataka kuona tunaandika historia nyingine katika msimu huu kwenye michuano hii mikubwa Afriká.”
Akizungumzia suala la Bonasi Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said alisema: “Huwa tuna kawaida ya kutoa Bonasi katika kila mchezo, lakini inatofautiana kiwango kutokana na umuhimu au ukubwa wa timu tunayokutana nayo japo utaratibu mzima ni siri ya uongozi na wachezaji.”