Kocha Mkuu wa Manchester United, Erik ten Hag, amesisitiza lawama za mwisho kwa timu yake kutolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa UIaya zinapaswa kuelekezwa kwake kama Kocha, lakini bado amekiri wachezaji pia wanastahili kụkosolewa.
United waliingia kwenye mchezo dhidi ya Galatasaray uliochezwa juzi usiku wakitakiwa kupata ushindi baada ya kupoteza michezo mitatu kati ya minne ya mwanzo katika hatua ya makundi.
Mambo yalianza vyema walipokuwa mbele kwa mabao 2-0, lakini Galatasaray ilitoka nyuma na kupata sare ya 3-3, licha ya Scott McTominay kuweka United mbele kwa 3-1.
“Ninawajíbika kwa hili,” alisema Ten Hag akiiambia TNT Sports.
“Tunajua tuko kwenye mradi, tunafanya maboresho, kwa hiyo nina matumaini makubwa. Tunaenda katika mwelekeo sahihi kwa hiyo najua tutafanikiwa kwa muda mrefu, lakini ukitaka kubaki Ligi ya Mabingwa Ulaya lazima kushinda michezo hii.
“Tulikuwa tunashinda halafu tunapoteza, tulipaswa kuchukua pointi tatu, hiyo ni wazi, tulifanya hivyo kwenye michezo mingine, nilifurahishwa na jinsi tulivyocheza lakini wakati huo huo lazima niikosoe timu kwa sababu ulinzi haukutosha.
“Tunaongoza 3-1 na hatuwezi kumudu makosa kwani inaleta mabadiliko.”
Nahodha wa United, Bruno Fernandes, pia akizungumza na TNT Sports, alikiri mabao waliyofungwa yalikuwa “mabaya sana” kutoka kwa mtazamo wa timu yake.
“Tulikuwa juu ya mchezo mara mbili na tulikuwa na nafasi nyingi sana za kufunga. Hatukuwa na umaliziaji mzuri,” alisema Fernandes.
“Sitaki kuwa hasi sana, lakini kile ambacho tumekuwa tukifanya kwenye Ligi ya Mabingwa hakitoshi, sio mchezo wa kwanza kuwa hivi, lazima tupate matokeo, lazima tuelewe aina hizi za michezo na hatua tunazopaswa kuchukua.
“Kila mtu anapaswa kuchukua hatua na kuwajibika kwa makosa yake mwenyewe.”