Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kimeanza safari ya kuelekea nchini Ghana, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko watatu wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Medeama SC.

Mchezo huo ambao utatoa mustakabali wa Young Africans katika Kundi D, umepangwa kuchezwa Ijumaa (Desemba 08) katika Uwanja wa Baba Yara mjini Kumasi, Mishale ya saa kumi na mbili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Kabla ya kuanza safari jijini Dar es salaam Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe alisema kikosi chao kinakwenda Ghana kwa matumaini makubwa ya kupambana na kupata ushiundi ugenini.

Amesema bado wanaamini Kundi D lipo wazi kwa timu zote shiriki, hivyo watapambana kwa nguvu ndani ya dakika 90, ili kufanikisha mpango wa kwenda Robo Fainali ya Michuano hiyo mikubwa Barani Afrika katika ngazi ya vilabu.

“Tunamshukuru mwenyezi mungu tumekuwa na maandalizi ya aina mbili kwa wachezaji wetu kabla ya kuanza safari yetu, Wachezaji walifanya mazoezi ya kurejesha miili sawa baada ya mchezo wetu dhidi ya Al Ahly, pia wachezaji walifanya mazoezi ya Gym.

“Wachezaji wote wapo salama, isipokuwa Joyce Lomalisa ambaye alipata majeraha katika mchezo uliopita, hivyo hatutakuwa naye katika safari yetu hii ya kuelekea Ghana. Tuna morari kubwa kwa ajili ya kwenda kupambana na kuwaletea matokeo mazuri mashabiki wetu.”

“Presha lazima iwepo kwa sababu tupo kwenye Michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa, na hii ni kutokana na ushindani uliopo katika hatua hii ya makundi, kila unapomaliza mchezo mmoja unapaswa kutambua mchezo unaokuja ni mgumu zaidi, kwa hiyo Presha ni kitu cha lazima na cha kawaida.” alisema Ally Kamwe

Young Africans inakwenda Ghana ikiwa inaburuza mkia wa Kundi D kwa kuambulia alama moja baada ya kucheza michezo miwili, ikipoteza mmoja dhidi ya CR Belouzdad na kutoka sare dhidi ya Al Ahly.

Medeama SC (Ghana) na CR Belouzdad (Algeria) zinalingana alama zote zikiwa na alama tatu, huku Al Ahly (Misri) akiwa kinara wa kundi hilo kwa kufikisha alama 4.

Uwajibikaji wa Sekta ya Madini Nchini waivutia Ghana
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 5, 2023