Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka nchini England Erling Haaland anaweza kuadhibiwa na Chama cha Soka nchini humo (FA), kwa kumkosoa mwamuzi, Simon Hooper, wakati Manchester City ikitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Tottenham Hotspur juzi Jumapili (Desemba 03) kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa X (zamani twitter).

Bao la kichwa la Dejan Kulusevski dakika ya 90 liliipa pointi Spurs, lakini City walinyimwa nafasi ya kushinda dakika tano baada ya zile za lala salama wakati mwamuzi Hooper aliposimamisha mchezo huku Jack Grealish akielekea kufunga kwa pasi ya Haaland.

Haaland alichezewa vibaya na beki wa Spurs, Emerson Royal, katikati ya uwanja, lakini akanyanyuka na kumpasia Grealish.

Mwanzo mwamuzi Hooper aliashiria faida kwa Man City kuendelea kushambulia, lakini kisha akapuliza filimbi wakati Grealish alionekana kuwa tayari kufunga.

Uamuzi huo ulizua hasira kutoka kwa Haaland, ambaye alioneshwa kadi ya njano na Hooper, lakini fowadi huyo wa Norway sasa yuko katika hatari ya kuadhibiwa na FA kwa chapisho lake kwenye X kwa kukiuka kanuni E3.1, inayosimamia maoni ya mitandao ya kijamii au matamshi yanayotolewa kwenye vyombo vya habari.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alishtakiwa na FA kwa maoni aliyoyatoa mwamuzi wa mechi kutokana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Newcastle mwezi uliopita. ESPN imewasiliana na FA kuuliza ikiwa Haaland pia atapokea adhabu.

Kocha wa City, Pep Guardiola alisema tukio hilo si sababu ya timu yake kupata sare kwenye mchezo huo, huku akimtetea Haaland. “Ni kawaida,” Guardiola alisema.

“Maoni yake yalikuwa yale yale kwa wachezaji 10. Kanuni ni kwamba huwezi kuzungumza na waamuzi au maofisa wanne, kwa hiyo tulipaswa kuwa na wachezaji 10 waliotolewa kwa kadi nyekundu. Amesikitishwa kidogo.

“Hata mwamuzi kama angeichezea Man City juzi angesikitishwa na kitendo hicho, hilo ni la uhakika.

“Nafanya makosa, wachezaji hufanya makosa. Erling alipoanguka, mwamuzi alisema cheza na baada ya kutoa pasi, alisimamisha mchezo.

“Sitaki kumkosoa, lakini hatukupata sare kwa ajili hiyo.”

Melis Medo atoa neno la shukurani Dodoma jiji
Waziri Mkuu awapa pole majeruhi Hanang'