Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amekabidhi Tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ kwa Baraza la Wanawake Wafugaji – PWC, Tanzania baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kati ya washindani 500 kutoka nchi mbalimbali dunia.

Tuzo hiyo, imetolewa na Taasisi ya Global Centre on Adaptation – GCA, jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu ambako unafanyika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), ambapo Kiongozi wa Baraza hilo kutoka jamii ya Kimasai, Maanda Ngoitiko ndiye aliyeipokea kwa niaba ya Baraza hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akikabidhi Tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ kwa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC) Tanzania, mshindi wa kwanza kati ya washindani 500 dunia.

“PWC wameiheshimisha sana Tanzania na kuifanya isikike duniani na nina uhakika kabisa tuzo hii imetokana na juhudi binafsi za dada yangu Maanda za kuimarisha uwezo wa uongozi wa wanawake wafugaji kwa kuwajengea uwezo kiasi cha kufikia usawa katika kutoa maamuzi katika jamii zao,” amesema Waziri Jafo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania wanaoshiriki Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) jijini Dubai.

Akishukuru kwa tuzo hiyo Bi. Maanda amesema kuwa Baraza hilo linawahudumia wanawake na wasichana kutoka jamii za Wamasai, Sonjo, Akie na Barabaig na kusema PWC ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi kaskazini mwa Tanzania kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo ya jamii kupitia uwezeshaji wa wanawake na wasichana wa Kimasai.

Tanzania, inaendelea kushiriki katika Mkutano wa COP 28 sanjari na mikutano ya pembezoni (side events), mikutano ya uwili (bilateral meetings) na warsha ambapo watu zaidi ya 81,000 kutoka nchi zaidi 190 wanahudhuria.

Erling Haaland mambo safi England
Rais mstaafu jela kwa kumiliki mali yenye mashaka