Ubalozi wa Marekani umetangaza kushirikiano na WiLDAF katika harakati za kutokomeza ukeketaji, kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Afrika – ARDF, ukifadhili mradi huo wa miezi 18 ujulikanao kama ‘Kutokomeza Ukeketaji mkoani Mara, Jamii Imara’ utakaotekelezwa mkoani Mara.

Mradi huo, unalenga kuchangia katika kuongeza kasi ya kutokomeza ukeketaji nchini Tanzania kama ilivyoainishwa katika Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ukeketaji, na utatekelezwa katika Wilaya tatu za Mara za Tarime, Butiama, na Serengeti.

Aidha, mradi huo wa ‘Jamii Imara’ pia utakuza maadili ya kijamii na kijinsia katika kutokomeza ukeketaji. Mradi utafanyakazi na vikundi vya wanawake na wasichana ili kuwawezesha kupata uelewa juu ya haki zao na masuala ya kijinsia.

Kwa wanawake na wasichana wasio mashuleni, mradi utajumuisha kipengele cha uwezeshaji kiuchumi, ili kutoa vyanzo mbadala vya mapato, kujenga uwezo wa kifedha na kupunguza uwezekano wa ukeketaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia.

Aidha, mradi wa Jamii Imara pia utafanya kazi na vijana wa kiume, viongozi wa kidini na kimila, ili kuwa mashujaa wa mabadiliko na kuongoza mipango ya mabadiliko ya kijamii katika ngazi za chini.

Katika ngazi ya kitaasisi, Jamii Imara itasaidia ujenzi wa mitandao imara ya asasi za kiraia na Serikali kwa ajili ya kujifunza kwa pamoja, kubadilishana uzoefu, kushirikiana na kuimarisha hatua za pamoja za kukomesha ukeketaji wa aina zote, ikiwa ni pamoja na mila zinazovuka mipaka.

Katika maadhimisho ya mwaka huu ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, mradi wa ‘Jamii Imara’ ni dhamira ya Serikali ya Marekani ya kuendelea kuwekeza na kusaidia asasi za kiraia na Serikali ya Tanzania katika mipango inayolenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Ushuru wa Vilevi uongezwe kupunguza vifo - WHO
Man Utd yamsaka mbadala wa Onana