Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa uboreshaji wa huduma za afya nchini hali iliyosababisha majeruhi wote wa mafuriko ya Hanang kupata huduma Mkoani Manyara, bila kupewa rufaa.
Dkt. Tulia ameyasema hayo mara baada ya kuwatembelea majeruhi hao hii leo Desemba 6, 2023, ambapo pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka utaratibu wa kuhudumia majeruhi wa maafa hayo.
Amesema, “nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuhudumia vyema majeruhi wa mafuriko na kutibiwa bure bila gharama yeyote.”
Aidha, Dkt. Tulia pia ameipongeza Wizara ya Afya na wataalamu wote kwa kazi nzuri waliofanya katika kuwahudumia majeruhi hao na kuwataka wataalam kuendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa Wananchi.