Afarah Suleiman, Hanang’ – Manyara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mikoa kuchukua tahadhari ya mvua, kulinda maeneo hatarishi na kufanya uchunguzi wa kina wa janga hilo ikiwemo kupatiwa makazi ya kudumu ya waathirika wote.
Rais Samia ametoa wito huo hii leo Desemba 7, 2023 mara baada ya kuwatembelea waathirika na majeruhi wa mafuriko katika mji wa Katesh, kabla ya kuzungumza na Wananchi wa eneo hilo huku akiyashukuru Makampuni na Mashirika yote yaliyo jitolea misaada mbalimbali.
Awali akimkaribisha Rais Samia, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wataendelea kuwahudumia Wananchi pamoja na kurejesha Miundombinu katika hali yake ya kawaida kwa kushirikiana na vyombo vya uli zi na usalama, Wananchi na mamlaka za Serikali.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema maafa hayo yamesababishwa na maporomoko ya tope kutoka katika mlima Hanang’ yaliyosoba mawe, miti pamoja na kuambatana na maji.
Naye Mkuu wa Mkoa Manyara, Queen Sendiga amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufika na kutoa pole kwa Wananchi wa Wilaya Hanang’ katika mji wa Katesh Mkoani humo.
Maafa hayo, yalitoke Desemba 3, 2023 na kusababisha vifo vya watu 76 na majeruhi 117 pamoja na kusimamisha baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji wa katesh uliopo Wilaya Hanang’ Mkoani Manyara.