Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema ni muhimu kwa nchi za Afrika kuweka mazingira bora ya biashara kupitia mfumo wa sera wezeshi zinazotambua changamoto za kipekee za Wanawake katika kurahisisha uendeshaji wa shughuli za kibiashara kwa wanawake.
Othman ameyasema hayo wakati akifunga Kongamano la pili la siku tatu la Wanawake katika Biashara katika eneo huru la Kibiashara bararani Afrika huko Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaama na kuhudhuriwa na Wafanyabiashara Wanawake kutoka nchi mbali mbali za Afrika.
Amesema, kufanya hivyo ni hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wa shughuli za kibiashara kwa wanawake sambamba na kuhakikisha uondolewaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kiushuru pamoja na kuweka mazingira sawa ya ushindani wa biashara ndani ya eneo huru la Biashara Barani Afrika.
Aidha, Makamu amesema hatua hiyo pia ni muhimu katika kuhakikisha uzalishaji wa ajira nyingi na zilizobora na hatimaye kuweza kuchochea mabadiliko ya haraka na kuwewezesha wanawake barani Afrika kushiriki kikamilifu katika shughuli za kibiashara na kuyafikia maendeleo endelevu kwa haraka.
Hata hivyo, Othman amefahamisha kwamba kufanyika kwa Kongamano hilo ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya nchi za Afrika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia ushiriki wao wa kibiashara ndani ya eneo huuru la Baiashara Barani Afrika.