Uchunguzi wa Idara ya Upelelezi – DCI, Nchini Kenya umebaini kuwa baadhi ya magari ya kifahari yamekuwa yakitumika kusafirisha dawa za kulevya, baada ya hivi karibuni gari aina ya Toyota Harrier kunaswa likiwa na kilo 477 za bangi, yenye thamani ya takriban Ksh. 14 Milioni kwenye barabara kuu ya Mombasa-Malindi.

Katika tukio hilo, watu wawili walikamatwa akiwemo George Nitti (37) na Raphael Mbithi (37), wakiwa katika eneo la Swallows, Kilifi Kusini kufuatia oparesheni iliyotekelezwa na Maafisa wa Polisi, wanaohudumu chini ya DCI.

Gari hilo lenye namba za usajili KDK 020B, lililokuwa likitumika kusafirisha dawa hizo haramu linashikiliwa na Polisi huku ripoti iliyowasilishwa katika Kituo cha Ndonya kilichopo eneo la Bunge la Kilifi Kusini, ikisema awali Dereva aligoma kusimamisha na kuwalazimu Polisi kufyatua risasi kwenye tairi la kulia.

Dawa hizo zilizonaswa na ambazo zilichunguzwa na Mkemia wa serikali Mombasa,zinakuwa si za mara ya kwanza kukamatwa kwenye magari ya kifahari ambayo yanatumika kusafirisha Dawa za kulevya, kwani Septemba 4, 2023 oparesheni nyingine ya DCI ilinasa gari jeusi aina ya Prado TX, lililokuwa likitumiwa kusafirisha Dawa hizo haramu.

Katika tukio hilo, kilo 316 za bangi zilizokadiriwa kuwa na thamani ya Ksh 9 milioni, zilipatikana baada ya gari hilo kupata ajali na kuangukia kwenye mtaro, huku wapelelezi wakipata nambari nyingi za usajili zinazofanana na zile zinazoonekana kwenye magari ya umma, jambo lilizua shaka zaidi.

Mwaka 2022 Rais wa Kenya, William Ruto, alitangaza vita dhidi ya walanguzi wa Dawa za kulevya na wauzaji mihadarati akiuhakikishia umma kwamba utawala wake utakabiliana na tatizo hilo katika eneo la Pwani, huku akiwaonya Wafanyabiashara wa Dawa hizo haramu kuondoka Nchini humo kabla ya hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Ukatili: Waathirika wa Ukoma wavunja ukimya
Jaribio la mapinduzi lamfikisha Rais mstaafu Polisi