Wakati Dirisha Dogo la Usajili Tanzania Bara msimu huu 2023/24, likitarajiwa kufunguliwa Desemba 16, mabosi wa Klabu ya Young Africans wameripotiwa kuwa katika hatua nzuri ya mazungumzo na uongozi wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini juu ya uwezekano wa kuinasa saini ya Mshambuliaji wa timu hiyo, Ranga Chivaviro.
Young Africans imekuwa ikitafuta mbadala wa Fiston Mayele aliyetimkia Misri katika Klabu ya Pyramid ambapo nafasi yake ilitarajiwa kuzibwa na Hafiz Konkoni, ambaye hata hivyo ameshindwa kuonesha makali yake ndani ya kikosi hicho hali iliyosababisha klabu hiyo kuelekeza nguvu zao katika kuisaka saini ya Chivaviro mwenye umri wa miaka 31.
Hata hivyo, licha ya uongozi wa juu wa klabu hiyo kuweka bayana kuwa suala la usajili ndani ya timu hiyo kwa sasa lipo chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, lakini imefahamika kuwa tayari mabosi wa timu hiyo wamekuwa na mawasiliano mazuri na viongozi wa Kaizer Chiefs juu ya uwezekano wa kumnunua mshambuliaji huyo ama kumpata kwa mkopo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kimeleza kuwa kwa sasa wapo katika mazungumzo ya kuona wanalimaza vipi na kumpata mshambuliaji huyo wa kati raia wa Afrika Kusini.
“Ni kweli tumekuwa na mazungumzo na viongozi wa timu ambayo anacheza huyo mchezaji kwa sababu bado nafasi ya mshambuliaji wa kati imekuwa tatizo na huyo mtu tunaona anaweza kutusaidia katika eneo ambalo tumeshindwa kupata dawa, kama kila kitu kikienda sawa basi tunategemea kuwa naye hapa,” alisema mtoa taarifa wetu.
Mtoa habari huyo alisema baada ya kufikia mapendekezo hayo, viongozi kupitia rais wa klabu hiyo, Hersi Said, alikuwapo Afrika Kusini kuzungumza na Kaizer Chiefs kwa ajili ya kuinasa saini ya nyota huyo.
“Kwa sasa hatua mshambuliaji mzoefu halisia na Kocha Gamondi amewataka viongozi kuanza na jambo hilo na tayari Hersi alifanya kikao na viongozi wa Kaizer Chiefs kwa ajili ya kumalizana na Chivaviro.
“Kikao hicho kimeenda vizuri na sasa imebaki hatua chache, ila haijafahamika vizuri ukubwa wa mkataba wake aliomalizana na Young Africans na muda atakaojiunga nao kambini, ila taarifa za uhakika ni kwamba Chivaviro atakuwa miongoni mwa nyota atakayecheza Young Africans,” amesema.
Ofisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema zoezi la usajili wa dirisha dogo wameshakamilisha na sasa wanasubiri kazi ya kutambulisha.
Amesema Kocha Gamondi tayari amekabidhi ripoti na tayari imeshafanyiwa kazi kwa kusajili mchezaji ambaye atakuja kuwa msaada kwenye timu ikiwamo safu yao ya ushambuliaji ambayo imefanyiwa kazi.
“Ni kweli tutafanya usajili kulingana na mapendekezo ambayo ameyaomba Gamondi, tayari kazi imefanyika, kwa Rais wetu Hersi kufanya kazi ya usajili mapema sana na tutashusha mtu hatari ambaye atakuja kukata kiu cha mashabiki wetu,” amesema Kamwe.