Baada ya kucheza michezo miwili ugenini ya Ligi Kuu Bara na kuvuna alama moja pekee, Tabora United imerejea mjini Tabora yalipo masikani yake kuendelea na ratiba zingine kuelekea michezo inayofuata.

Ofisa habari wa Tabora United, Pendo Lema, amesema, tayari kikosi kipo imara na mazoezi yameanza kujifua kuelekea michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ambapo Jumamosi (Desemba 16) watacheza dhidi ya Monduli Coffee.

Pendo amesema kupoteza alama tatu dhidi ya lhefu FC siyo kupoteza malengo ya klabu.

“Tumewasili salama nyumbani tukitoka Mbeya ambapo tulikuwa na michezo miwili ya ugenini, mmoja tumecheza Lake Tanganyika pale Kigoma dhidi ya Mashujaa FC ambapo tulifanikiwa kuondoka na alama moja baada ya sare ya 1-1, mchezo wa pili tukapoteza dhidi ya Ihefu kule Mbeya.

“Mchezo uliopita tumepoteza alama tatu, lakini hatujapoteza malengo yetu, Tabora United bado tuna matamanio makubwa na bado hatupo katika nafasi nzuri kwa upande wetu, hivyo tunapambana kufikia malengo yetu mwisho wa msimu.

“Kikosi kimeanza mazoezi kujiandaa na mashindano ya ASFC ambapo katika mashindo haya tumepangwa kucheza na Monduli Coffee ya Arusha.

“Tutatumia Uwanja wa Jamuhuri Dodoma kama uwanja wetu wa nyumbani na hii ni kutokana na kuwa uwanja wetu unaendelea kufanyiwa ukarabati,” amesema Lema.

Ahmed Ally: Nina imani kubwa na Benchikha
Mafuriko Hanang': NBC wakabidhi misaada, fedha taslim