Benki ya Taifa ya Biashara – NBC imekabidhi msaada wa fedha taslimu kiasi cha Sh milioni 10, Chakula, Nguo na Mablanketi kwa waathiirika wa mafuriko vyenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 20, Wilayani Hanang’, Mkoani Manyara.
Msaada huo, umekabidhiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa benki hiyo, Godwin Semunyu kwa kushirikiana na Wafanyakazi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Semunyu amesema NBC inatoa salamu za pole kwa waathiirika wa tukio hilo, Serikali na Watanzania kwa ujumla na kwamba imepokea kwa huzuni kubwa taarifa za athari zilizotokana tukio hilo ikiwemo vifo na upotevu wa mali.
Amesema, Benki hiyo inaungana na watanzania kwa ujumla katika kuwafariji wahanga wa tukio hilo kwa hali na mali na zaidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wote waliojeruhiwa na waliopoteza maisha katika janga hilo.
Akipokea msaada huo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jimmy Yonaz aliishukuru benki hiyo kwa kuguswa na kuwafikia wathirika hao wa mafuriko kwani inathibitisha nia ya dhati waliyonayo katika kushirikiana na jamii.
Aidha ameziomba Benki na Taasisi mbalimbali za umma na binafsi kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwasaidia waathiirika hao waliokubwa na mafuriko kufika katika mji wa katesh wilayani Hanang’ Mkoani Manyara.