Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.
Katibu Mtendaji wa kanda ya Afrika Mashariki wa Pan African Women Organization – PAWO, Dkt. Suzan Kolimba amewataka Wanawake wenye sifa za kuwa Viongozi, kuanza maandalizi ya kugombea nafasi mbalimbali katika chaguzi za Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi Mkuu wa 2025, ili wasaidie Taifa kupiga hatua za maendeleo.
Dkt. Suzan ameyasema hayo mjini Kibaha Mkoani Pwani, wakati akihutubia Wanawake Viongozi Vijana kutoka nchi 20 za Afrika katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu huo akimuwakilisha Rais wa PAWO, Eunice Ipinge na kuongeza kuwa ni vizuri Wanawake wakashiriki kugombea nafasi hizo za uongozi.
Amesema, “kundi la Wanawake ni waaminifu katika kuongoza kwani wanajituma, hivyo nawahamasisha Wanawake inapofika mwaka 2024 kwa chaguzi za serikali za mitaa na hata serikali kuu mwaka 2025 wakachukue fomu wagombee ili washike nafasi watuongoze wasaidie kutoa mchango mkubwa badala ya kuishia tu kusema kuna wanaume hawa wanatutawala.”
Dkt. Suzan ameongeza kuwa, kabla ya ukoloni Wanawake walikuwa na haki na wajibu wa kupewa nafasi ya kuongoza huku akimtolea mfano Bibi Titi Mohamed, ambaye alipambana licha ya ubanaji wa uhuru wa Wanawake kwa kipindi hicho na kusema Wanawake wengine walikuwa Machifu na waliongoza vizuri ingawa kulikuwa na mipaka na uhuru wa nafasi zao.
“Hii Pan African Women Organization ilianzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias kambalage Nyerere mwaka 1962 hapa Tanzania, Dar es salaam kwa kushirikiana na vyama 11 vya nchi za Afrika ambapo walifanya m kutano wa kwanza wa wanawake viongozi ambao ndio ulitengeneza msingi, mwelekeo wa nguvu ya mwanamke kuwasaidia wanaume kuweza kupambania uhuru wa nchi zetu,” alisema Dkt. Suzan.
Naye Mratibu wa Mkutano huo, Precious Banda kutoka Afrika Kusini alisema wanaipenda Tanzania kwani ni nchi ya muasisi wa taasisi hiyo, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere, ambaye alitaka Wanawake Vijana Viongozi wa nchi za bara zima la Afrika waungane kusaidia harakati za ukombozi wa nchi zao na kufanikisha hatua maendeleo katika mataifa yao.
Mkutano huo Mkuu wa mwaka, umehusisha Viongozi Wanawake Vijana wanaotoka katika katika vyama vinavyoongozwa na Viongozi Wanawake wa nchi 20, ikiwemo Kenya, Tanzania, Namibia, Zimbabwe, Rwanda, afrika ya kusini, Angola, Zambia, Madagaska, Uganda na Swaziland.