Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema hana presha na mchezo ujao wa Ligi kuu Tanzania Bara, licha ya kuwa na matokeo mabaya yanayomkabili, huku akidai kuwa hawaiogopi Young Africans.

Mtibwa Sugar itakuwa ugenini jijini Dar es salaam, Jumamosi (Desemba 16) dhidi ya Young Africans ambao wanarudi kwenye Ligi Kuu baada ya kukosekana kwa muda kutokana na kubanwa na ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katwila aliyejiunga na timu hiyo mwezi Oktoba, mwaka huu akitokea Ihefu FC, ameiongoza katika mechi sita na kushinda moja, amesema kuwa wanaendelea na maandalizi kuhakikisha kikosi kinarudi kwenye ushindani bila kujali wanakutana na timu gani.

Kocha huyo amesema timu yake haina mwenendo mzuri hivyo ni lazima afanye kazi ya ziada kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa bila kuhofia mshindani wao, huku akisisitiza kuwa mbinu na maandalizi bora ndivyo vitakavyoamua matokeo.

“Tutaingia kwa kuwaheshimu Young Africans Jumamosi (Desemba 16) na siyo kuwaogopa tunacheza na timu yenye wachezaji 11 kama sisi na changanmoto tunayoipitia ni kipindi cha mpito timu nyingi huwa zinapitia nyakati ngumu kama hizi matokeo haya hayanifurahishi, nimeandaa programu nyingine za mazoezi na kuwapa wachezaji muda zaidi wa mazoezi wa kuongeza viwango vyao,” amesema.

Kocha huyo amesema anataka kuiona Mtibwa Sugar ikiendelea kushiriki Ligi Kuu na kupanda juu katika msimamo.

Katika msimamo, Mtibwa Sugar inaburuza mkia ikiwa na pointi tano baada ya kushuka dimbani mara l2.

Kocha huyo aliiongoza Mtibwa Sugar kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Geita Gold kabla ya kufungwa bao 1-0 na KMC kisha kupoteza 2-1 ilipocheza na JKT Tanzania na kukubali kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Azam FC huku ikikubali kufungwa mabao 2-1 na Tabora United kisha kuchapwa bao 1-0 na Namungo FC.

Watendaji Dawati la jinsia ongezeni juhudi - CP Kaganda
Kliniki ya Ardhi: Hati Miliki 3,156 zatolewa kwa Wananchi