Kocha wa viungo, Shadrak Nsajigwa na Mrundi, Vladimir Niyokuru wamekabidhiwa kwa muda kikosi cha Namungo FC, baada ya kuondoka kwa Kocha Denis Kitambi.

Uongozi wa Namungo FC umethibitisha kuikabidhi timu kwa makocha hao, baada ya kuachana na Kocha Kitambi ambaye ameshindwa kuendelea na kazi klabuni hapo, kwa kushindwa kufikia makubaliano ya kimaslahi.

Ofisa Habari wa Namungo FC, Kindamba Namlia, amesema wameachana na kocha huyo baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili, lakini wanamshukuru kwa muda wote aliokuwa katika kikosi chao kinachoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tunamtakia kila la kheri Kocha Denis Kitambi katika safari yake ya ukocha nje ya Namungo FC,” amesema Namlia.

Hata hivyo inadaiwa kuwa Kocha huyo mzawa yupo katika mazungumzo na Uongozi wa Ihefu FC, ambayo imekuwa ikisaka Kocha Mkuu, baada ya kuachana na Kocha kutoka nchini Uganda Moses Basena.

Imeelezwa awali, Ihefu FC ilikuwa inamhitaji Juma Mgunda, lakini imeshindikana kutokana na kocha huyo kuwa na mkataba na Simba SC akiwa na cheo cha Mkurugenzi wa Ufundi, akihudumu hasa katika timu za vijana na Simba Queens.

Young Africans kushusha vyuma Dirisha Dogo
Majaliwa awapigia chapuo Madereva wa Malori