Tabora United ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Kitayosce FC imeingia katika mkumbo wa kufungiwa kusajili na Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’, baada ya kushindwa kumlipa stahiki zake mmoja wa wachezaji waliowahi kuitumikia klabu hiyo.

Taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ imemtaja Ngoywangoy Fabrice kuwa chanzo cha Klabu hiyo ya mkoani Tabora kufungiwa kusajili, katika kipindi hiki cha kuelekea Dirisha Dogo.

Uamuzi huo umefanywa na Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ baada ya mchezaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.

Ngoywangoy Fabrice, aliishtaki Tabora United FIFA kwa madai ya kutolipwa malipo ya malimbikizo ya mishahara.

Hata hivyo Tabora United, ilitakiwa na ‘FIFA’ iwe imemlipa mchezaji huyo ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini haikutekeleza hukumu hiyo.

Wakati FIFA ikiifungia Tabora United kufanya usajili wa Wachezaji wa Kimataifa, Shirikisho la Soka ‘TFF’ limeifungia kufanya usajili wa ndani.

Katika hatua nyingine TFF imezikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na Wachezaji pamoja na Makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.

Mgunda: Tunautaka ubingwa Ligi Kuu
Ukatili: Polisi yaelimisha uchangiaji damu