Mabosi wa Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro wamekubali kumuachia Kiungo wao Mshambuliaji, Ladack Chisambi kwa sharti la kutoa kitita cha Shilingi MIlioni 8o ili asaini Simba SC.
Kiungo huyo ni kati wachezaji waliokuwepo katika rada za Simba SC katika usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa Ijumaa (Desemba 15).
Usajili wa kiungo huyo unakuja kuiboresha timu hiyo, inayoshiriki michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Mmoja wa viongozi wa Mtibwa Sugar, amesema kuwa uongozi wao hauoni sababi ya kumng’angania kiungo huyo, badala yake umetoa baraka za kumuachia Chasambi mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.
Kiongozi huyo amesema kuwa wapo tayari kumuachia kiungo huyo kwa sharti la kuuvunja mkataba wake wa miaka mitatu kwa dau la Shilingi Milioni 80.
Ameongeza kuwa fedha hizo za usajili zitatumika kwa ajili ya kumpata mbadala wake mwenye kiwango kikubwa katika dirisha hili dogo la usajili msimu huu 2023/24.
Amesema kuwa wamepanga kukiboresha kikosi chao katika dirisha hili dogo kwa kuwasajili wachezaji wenye uzoefu watakaoibakisha timu Ligi Kuu Bara.
“Mtibwa Sugar hatuna utamaduni wa kumzuia mchezaji kwenda kucheza kwingine, kikubwa tunachokiangalia ni maslahi pekee ambayo timu itanufaika nayo.
“Hivyo tutamuachia Ladack kwa sharti la timu itakayomuhitaji kutoa dau nono la usajili katika dirisha dogo,” amesema kiongozi huyo.
Mtendaji wa Simba SC, Imani Kajula hivi karibuni alizungumzia suala hilo la usajili kwa kusema kuwa: “Ni lazima tufanye katika usajili huu wa dirisha dogo, kwa lengo la kuboresha kikosi chetu, lakini suala lote usajili lipo kwa kocha wetu Benchikha (Abdelhak).”