Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Dickson Job, amewataka wachezaji wa Mtibwa Sugar kupambana na kuipigania timu hiyo inayoburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuepuka janga la kushuka daraja.

Ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Manungu Complex ulioko Turiani, Morogoro juzi Jumanne (Desemba 19) Mtibwa Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC, lakini matokeo hayo hayajawanasua kutoka mkiani.

Job amesema Mtibwa Sugar ni moja ya timu kubwa nchini na haitakuwa vyema kuiona klabu yake hiyo ya zamani ikienda kushiriki Ligi ya Championship msimu Ujao 2024/25.

Beki huyo ambaye hakucheza mechi ya Jumamosi (Desemba 16) dhidi ya timu yake hiyo ya zamani, aliwataka wachezaji wa Mtibwa Sugar kuamka na kujituma, ili kusaka matokeo mazuri yanayoweza kuwanusuru na balaa hilo.

“Mtibwa Sugar ni timu kubwa ambayo imetoa wachezaji wakubwa na wenye heshima nchi hii. Kikubwa ninawaomba waendelee kupambana, wachezaji wote wajitoe, Mtibwa imetoa nyota wengi, achana na sisi wa miaka ya karibuni.

Kuna wachezaji waliofanya mambo makubwa waliwahi kupitia hapa, haitakuwa vyema kwa macho yetu tukiiona inashuka, hatutajisikia vizuri,” amesema Job.

Kabla ya kupata ushindi huo wa juzi, Jumamosi (Desemba 16) iliyopita Mtibwa Sugar ilipata kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Young Africans, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.

“Naamini wanapitiwa na wakati mbaya tu, angalia katika mechi yetu wamecheza vizuri tu, ni matatizo madogo madogo sana yanawasumbua, watarudi kwenye nafasi waliyoizoea, amesema Job ambaye alijiunga na Young Africans mwaka 2021 akitokea Mtibwa Sugar.

Mtibwa Sugar ambayo imekuwa na misimu mibaya mitatu mfululizo, imejikusanyia alama nane katika michezo 14 ambayo imecheza msimu huu.

Julio akubali uwezo wa Benchikha
Benchikha atoa neno Simba SC