Klabu ya Medeama SC ya nchini Ghana imefikia uamuzi wa kumuondoa katika nafasi ya Ukocha Mkuu, Evans Adotey aliyekuwa anakinoa kikosi hicho katika msimu huu.
Maamuzi hayo yamekuja ikiwa ni siku moja imepita tangu, Medeama SC itoke kuchezea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Young Africans mchezo uliopigwa Jumatano (Desemba 20) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Katika mchezo huo ambao, Young Africans walitawala dakika zote 90, mabao yao yakifungwa na kiungo fundi Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Mudathiri Yahya.
Evans mwanzoni mwa msimu huu aliajiriwa kama Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo kabla ya kubadilishiwa majukumu na kuwa Kocha wa muda kutokana na kutimuliwa kwa David Duncan aliyekuwa akibudumu katika nafasi hiyo.
Hivyo hivi sasa Evans atasalia kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Medeama SC na siyo Kocha Mkuu wa Muda kama ilivyokuwa awali.
Kocha huyo aliiongoza timu hiyo, na kufanikiwa kuwafunga CR Belouizdad bao 1-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulipigwa Ghana.
Pia Kocha alifanikisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Young Africans ambayo ilionekana kucheza katika kiwango bora kwenye mchezo wa awali, uliopigwa Ghana kabla ya kuja kurudiana Uwanja wa Benjamin Mkapa na kufungwa mabao 3-0.