Wafanyabiashara Nchini, wametakiwa kuhifadhi bidhaa zao vizuri ikiwemo kuziweka katika vifaa salama, ili kulinda afya zao, za wateja na jamii kwa ujumla.
Wito huo, umetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Gairo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Happiness Laizer wakati akizungumza na Wafanyabiashara mbalimbali katika gulio la Kata ya Rubeho Wilayani Gairo Mkoani Morogoro.
Amesema, “bidhaa hizi zinatumiwa na watu wengi hasa kama chakula kwaiyo ni jukumu lenu kuziweka na kuzihifadhi katika mazingira mazuri ili kuweza kulinda afya za wateja wenu.”
Aidha, SSP Laizer amewataka wafanyabiashara hao kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi na kuimarisha ulinzi, ili iwe rahisi kuzuia uhalifu wawapo kwenye biashara zao.
Wafanyabiashara hao pamoja na waendesha bodaboda pia walipewa elimu ya ukatili wa kijinsia, ambapo walielezwa maana na aina zake na kutakiwa kuwa mstari wa mbele kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.