Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Twaha Kassim ‘Kiduku’, amesema amejipanga vyema kumchakaza mpinzani Mohamed Sebyala kutoka Uganda katika pambano litakalofanyika leo Jumanne (Desemba 26).

Kiduku atazichapa na Sebyala katika pambano la Raundi 10, kuwania mkanda wa PST uzito wa juu, litakalofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, bondia huyo amesema amejiandaa vizuri kufunga mwaka kwa kuwafurahisha Watanzania.

“Namshukuru Mungu nipo salama, nimefanya mazoezi ya kutosha, pambano litakuwa gumu kwa sababu mpinzani ni mzuri na mgumu kupigika, lakini nimejiandaa vizuri kumpiga,” amesema.

Kocha wa Bondia huyo, Pawa Iranda aliweka wazi kuwa Kiduku atatumia pambano hilo kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika pambano lililopita, ambapo Mtanzania huyo alipoteza kwa pointi dhidi ya Asemhle Welleh kutoka Afrika Kusini.

Kwa upande wa Sebyala, amesema anaamini pambano hilo litakuwa zuri kwa kuwa anakutana na mpinzani mwenye ubora, lakini atatumia uzoefu wake kuonyesha kiwango bora.

“Nawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kwani watafurahi, Kiduku ni bondia mzuri, lakini mimi nimecheza na wakubwa wake kama Rashidi Matumla na wengine,” amesema.

Mbali ya pambano hilo, mabondia wengine watakaopambana ulingoni leo Jumanne (Desemba 26) ni mzawa Oscar Richard dhidi ya Sabelo Ngebinyana kutoka Afrika Kusini, wakati Tampera Maurusi akizichapa na Waziri Magombana.

Said Torres atavaana na Richard Mkude, Charles Tondo dhidi ya Nick Otieno wa Kenya, huku Sara Alex atapigana na Jesca Mfinanga.

 

Salah: Hatutakubali kuangusha alama kizembe
Mikel Arteta aahidi makubwa 2024