Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amesema Young Africans ndio timu inayompa wakati mgumu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu 2023/24.
Akizungumza jijini Dar es salaam kocha huyo kutoka nchini Senegal amesema kitendo cha Young Africans kushinda mfululizo kinampa wakati mgumu na kujikuta wanacheza mechi zao kwa Presha kubwa.
“Kitendo cha Young Africans kushinda mechi zao za viporo kinatupa Presha sababu kama wataendelea kushinda watatuzidi na kuwa juu yetu kitu ambacho kinafifisha matumaini yetu ya ubingwa,” amesema Dabo.
Kocha huyo amesema pamoja na changamoto hiyo ataendelea kupambana na wasaidizi wake ili kuhakikisha hawafanyi makosa katika kila mechi watakazocheza za ligi.
Amesema anajivunia ubora wa kikosi chake kwa sasa tofauti na walivyoanza msimu lakini hawatobweteka wataendelea kupambana ili kupata matokeo mazuri mfululizo kama wanavyofanya sasa.
Azam FC ipo kileleni mwa msimamo wa ligi, ikiwa na alama 31 katika michezo 13 wakifuatiwa na mabingwa watetezi Young Africans walio na alama 30 katika michezo 11.