Baada ya dili lalke la usajili kukamilika kwa asilimia mia moja, kiungo mpya wa Simba SC, Ladack Chasambi anatarajiwa kukiongoza kikosi hicho katika Kombe la Mapinduzi katika msimu huu.
Chasambi ni kati ya wachezaji wapya waliokuwa wanawindwa vikali na baadhi ya klabu za hapa nchini kutokana na kiwango bora ambacho anakionyesha akiwa anaichezea Mtibwa Sugar ya Turiani, Manungu mkoani Morogoro.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kufanyika keshokutwa Alhamis (Desemba 28), kisiwani Unguja, Zanzibar.
Taarifa zinaeleza kuwa kuwa kiungo huyo dili lake limekamilika kwa asilimia mia moja ndani ya Simba SC, kilichobakia kwake ni kutambulishwa pekee.
Mtoa taarifa huyo amesema kuwa kiungo huyo mara baada ya kutambulishwa rasmi ataanza kuichezea timu hiyo katika Kombe la Mapinduzi 2024.
Ameongeza kuwa kiungo huyo anatarajwa kuwepo katika msafara wa timu hiyo, utakaosafiri kwenda Zanzibar ndani ya siku hizi mbili kujiandaa na michuano hiyo.
“Ladack usajili wake umekamilika kwa asilimia kubwa, na yeye huenda akawa mchezaji wa kwanza kutambulishwa katika timu.
“Pia kiungo huyo anatarajwa kuanza kuichezea timu hiyo, katika Kombe la Mapinduzi ambalo wamethibitisha kushiriki katika msimu huu 2023/24.
“Kiungo huyo amesajiliwa baada ya kufikia makubaliano mazuri na Mtibwa Sugar ambayo tumemnunua kwa mkataba wa miaka mitatu,” amesema mtoa taarifa huyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally alisema kuwa: “Tumepanga kukifanyia maboresho makubwa kikosi chetu kupitia usajili huu wa dirisha hili ambao umefunguliwa hivi karibuni.”